10 Mei 2025 - 22:05
Source: Parstoday
Pakistan yaanzisha operesheni ya kijeshi ya "Al-Bun-yan Al-Marsoos" dhidi ya India

Baada ya India kufanya mashambulizi makubwa ya anga, jeshi la Pakistan limeamua kulipiza kisasi kwa kuanzisha mashambulizi ya anga, ya makombora na maroketi dhidi ya maeneo ya India. Operesheni hiyo imepewa jina la Al-Bun-yan al Marsoos yaani Jengo Lililoshikamana. Sambamba na kuanza operesheni hiyo, taarifa zinasema kuwa kumefanyika mashambulizi makubwa ya mtandao dhidi ya gridi ya umeme ya India.

Mapema leo Jumamosi asubuhi, serikali ya Pakistan imetangaza habari ya kuanzisha operesheni kubwa ya kijeshi iitwayo "Al-Bun-yan Al-Marsous" dhidi ya India.

Hatua hiyo imechukuliwa kujibu mashambulizi ya anga ya India kwenye kambi tatu za kijeshi za Pakistan saa chache zilizopita. Kwa mujibu wa televisheni rasmi ya Pakistan, vituo vyote vya kijeshi vya Pakistan viko salama na havikuathiriwa na mashambulizi hayo ya India.

Jeshi la Pakistan limetangaza kuwa, limeshambulia vituo vya anga vya Pathankot na Udhampur nchini India, pamoja na ghala la makombora katika eneo la Beas.

Mashirika ya habari yameripoti kutokea miripuko mingi katika miji ya Amritsar na Jammu nchini India. Shirika la habari la Reuters limeripoti kutokea miripuko isiyopungua sita katika mji wa Srinagar katika jimbo la Kashmir.

Pakistan imefunga kwa muda anga yake kwa safari zote za ndege za kuingia na kutoka nchini humo. Hatua hiyo imechukuliwa ili kuimarisha usalama wa ndege na kuzuia vitisho vyovyote vinavyoweza kutokea. Pia kumekuwa na ripoti za usumbufu mkubwa wa gridi ya umeme nchini India.

Kwa mujibu wa televisheni ya Pakistani, takriban asilimia 70 ya gridi ya umeme nchini India imepata matatizo kutokana na mashambulizi ya mtandaoni. Kwa upande wake, India imetangaza kuwa imefanikiwa kuangusha karibu asilimia 70 ya droni yaani ndege zisizo na rubani zilizorushwa kutokea Pakistan. Wasiwasi umeongezeka kutokana na nchi hizo mbili kumiliki silaha za nyuklia.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha